Sunday, 19 October 2014

PONA KWA IMANI YAKO ILA USIDANGANYIKE

PONA KWA IMANI YAKO ILA USIDANGANYIKE
Joseph Julius(MD, MUHAS)

“Ona!imani yako imekuponya”,ndivyo yesu alivyomwambia kipofu mmoja huko yeriko baada ya kupona upofu. Hapa alikua sawa kabisa,imani inaponya kweli. Kinachonisikitisha na kunisumbua mimi kama mwanafunzi wa tiba ya kisayansi na ya kisasa ya wanadamu ni jinsi gani uwezo huu wa imani kuponya ulivyovamiwa na waganga wa jadi pamoja na viongozi wa dini,ambao sintosita kuwaita matapeli.

Ndio maana Kwenye mashahiri ya chekacheka T.mvungi hakusita kuuburuza wino karatasini kwamba:
                      
                         Kimbilio la wanyonge,limejigeuza chatu,
                         Chatu mmeza matonge,asieogopa watu,
                         Dawa uchonge singe,chatu afanywe si kitu,
                         Akishaoza samaki,busara ni kumtupa.

Naam,na tuzichonge singe zetu basi,kwangu mimi singe ni elimu,tufahamu nini maana ya kupona kwa imani ili kuepusha kutapeliwa basi huko mbele na labda kuokoa maisha ambayo huenda yangeokolewa kwa njia nyingine ila sio lazima iwe hii ya imani.

Kwanza kabisa tutambue kuwa miili ya wanyama ina mbinu asilia za kuepukana na kujitibu magonjwa,hii nitaiita kinga asilia dhidi ya magonjwa. Tunatapika tukila vitu vibaya ili kusafisha mfumo wa chakula wa juu,tunaharisha kusafisha mfumo wa chakula wa chini,jotoridi letu la mwili likipanda(homa) ,miili yetu inapambana vizuri zaidi na maambukizi. Mbinu zote hizo pia zinaweza kumgharimu mnyama hata maisha yake pia. Sote tunajua athari za kuhara au kutapika kupita kiasi au kwa muda mrefu. Kwa hiyo sasa, miili ya wanyama ipo makini sana katika kuruhusu mbinu hizo zifanye kazi.

Wengi tunafaham pia kuwa kama tukipata tetekuwanga mara moja maishani basi hatutopata tena na pia hata malaria inapunguza kutusumbua kadiri tunavyozidi kuwa wakubwa ukilinganisha na utotoni.
Hapa kinachotokea ni kwamba: vimelea vya maambukizi vikishaingia kwenye miili yetu,miili yetu inavitambua na kutengeneza vitu mfano wa askari ambao watapambana navyo kama vitakuja kuvamia tena.

Kama vimelea hivyo vitarudi na sura ileile basi vitatambuliwa na kuchukuliwa hatua za haraka na hatutapata ule ugonjwa. Vimelea navyo vijanja lakini,huwa vinarudi vimebadilisha sura kitu ambacho kinaulazimu mwili kutengeneza askari wengine watakaoweza kuvitambua tena. Kwa hiyo usipende kwenda maabara kupima malaria ukaambiwa “una ringi mbili za malaria” nawe ukaenda kubugia dawa,ni kawaida kuwa na hivyo vimelea kwenye damu kama unaishi haya maeneo yenye maambukizi mazito,lakini haimaanishi unaumwa;sanasana utapelekea mwili wako kuwa sugu kwa dawa hizo na siku ukiumwa kweli ikawa shida kukutibu.

Nilichokieleza hapo juu ndio sababu za magonjwa hasa ya watoto huwa yanapona bila hata kuwafikisha hospitali japo jamii inaamua kuweka imani zake,kwa mfano wanasema watoto huwa wanalilia majina ya mababu/mabibi/mizimu na ukiwabadilishia wanaacha kulia. Wanaongeza kuwa ukikosea jina wataendelea kulia tu na inabidi ubadilishe ili uone,wanaongeza tena kuwa kama mtakosea jina basi kitoto kitalia mpaka kufa. Hapo wamekosea; kipindi kitoto kikiacha kulia basi kinga asilia imefanya kazi na kama ndio walikua wamebadilisha jina basi matukio mawili yameenda pamoja ila moja(la jina) halina matokeo,na kama itashindwa basi kitoto kitahangaika mpaka kufa na watatafasili kimekataa jina.

Turudi basi kwenye imani kuponya; ili kukufungua macho acha nikuelezee kuhusu “placebo effect” kwanza; kwenye kamusi yangu ya TUKI(eng-swah) neno placebo limetafsiriwa kama kipozauongo:dawa ya kutuliza/kupoza,ila kama tutakavyokuja kuona hapo baadae hii sio dawa.
Wataalam wa tiba wakiwa wanataka kujua kama dawa au mbinu Fulani ya tiba inatibu kweli huwa wanatumia kipoza uongo kwa upande mmoja na dawa au mbinu inayochunguzwa kwa upande mwingine,kipozauongo hicho hufanana sana na ile dawa ila tu inaondolewa kiambato muhimu ambacho ndicho kinasemekana kuponya.

Mfano tunataka kuchunguza kama dawa fulani iliyotengenezwa kwa ajili ya kutibu malaria kama kweli inatibu malaria,tutachukua wagonjwa waliothibitishwa kuwa na malaria na tutawagawa katika makundi mawili bila wao kujua,tuseme wapo elfu moja kila kundi. Alafu tutachukua ile dawa inayosemekana inatibu malaria kutokana na kuwa na kiambata Fulani kiitwacho X labda,alafu tutatengeneza kidonge kingine kama hiyo dawa na tutaiondolea kiambata X ila itafanana kabisa na ile dawa ya kweli kwa vitu vingine vyote(hii ndio kipozauongo)

Baada ya hapo tutaligawia kundi moja la wagonjwa dawa inayojaribiwa na jingine kipozauongo katika kipimo na masharti sawa. Baadae tutakuja kuchunguza idadi ya wagonjwa waliopona kutoka katika kila kundi. Kila kundi litakua na wagonjwa waliopona na ambao hawajapona. Ili dawa/mbinu ile inayojaribiwa ionekane kuwa ni kweli inaponya,namba ya waliopona lazima ivuke kiwango flani cha kitwakwimu,kwa mfano wale waliopewa dawa wanaweza kupona kwa 99.9% na lile kundi lililopewa kipozauongo wakapona 1%.
Je hawa waliopona bila kupewa dawa wameponaje?imani yao imewaponya,kuna uhusiano kati ya saikolojia na fiziolojia ya mwili.
Wenzangu na mimi wanaosoma/wanaofanya tiba watakubaliana na mimi kuwa kuna umuhimu wa kutengeneza ukaribu kati yako na mgonjwa,kuwa sehemu ya kinachomsumbua,jinsi ya kujionesha mbele yake,na mengine. (Angalia hapa pia)

Nakumbuka tukiwa wodi ya wazazi,ukiwasogelea wajawazito walio karibu kujifungua ukawa unawapa moyo kwa kuwashika mkono na kuwaaminisha kuwa haitakuwa shida wanaonekana kupunguza kuhangaika na wanatulia kama maumivu yamepungua.

Baba wa udaktari Hippocrates aliwahi kusema ”watu wanadhani kifafa kimeshushwa toka mbinguni,kwa sababu tu hawakielewi. Ila kama wangeita kila kitu wasichokielewa kuwa kimeshushwa,basi vitu vilivyoshushwa visingekuwa na mwisho”. Kupona kwa imani kunatokea kwa uwezekano mdogo sana ukilinganisha na tiba zilizowahi kufanyiwa utafiti kisayansi na zinazotolewa na watu waliotumia miaka mitano au zaidi wakijifunza sababu za magonjwa,jinsi magonjwa yanavyoathiri mifumo wa mwili,vipimo vya kuhakiki na hatimaye tiba,kuzuia na ushauri.

Inasemekana miaka mia hamsini iliyopita bikira la Maria alimtokea mtakatifu Bernadete Soubirous huko Lourdes,Ufaransa mara kumi na tatu na tangu hapo watu huenda kuhiji huko. Tovuti ya www.catholicnews .com imendika kwamba zaidi ya watu milioni sita huenda kuhiji huko kila mwaka wakiomba kuponywa na msamaha. Ila watu sitini na saba tu ndio waliorekodiwa kuwahi kupona kati ya hayo mamilioni,hii ni kipozauongo. Yale tunayoyaona kwenye runinga kuwa makundi makubwa ya watu yanapona palepale baada ya kuombewa,tena magonjwa makubwa kabisa kama saratani na UKIMWI ni ghilba tu ya kutaka kuvuta wateja wengi zaidi. Nakumbuka kichekesho cha mtu aliekuwa kipofu toka amezaliwa ila baada ya kuombewa na kuona aliweza kuzitambua rangi za simba na yanga.

Ni vyema basi tukipata magonjwa kuanzia kwanza kwenye tiba hii ya kisasa,tiba ya kisayansi,tiba ya magharibi kama inapatikana kabla ya kwenda huko kwingine kwa sababu kama tulivyoona kuna uwezekano mdogo sana wa kipozauongo kukuponya(japo inawezekana). Waganga wa kienyeji wao hutoa hata dawa za kunywa ambazo hazijafanyiwa utafiti na hivyo madhara yake hawayajui,hizi huweza kusababisha matatizo ya figo. Ila nisiwaonee waganga wa kienyeji tu,siku hizi hata viongozi wa dini nao wanatoa vitu vya kumeza kama dawa walizooneshwa na mungu wao,nikitaja neno Roliondo sihitaji kuelezea zaidi kilichotokea. Umaskini wetu unafanya iwe ngumu kuipata tiba hii ya kisasa ila hilo halimaanishi siyo ya kweli.kwa mfano kuna magonjwa ambayo ili wapate tiba yake ni lazima upigwe picha ya MRI labda,hizi zipo chache na wengi wetu hatuwezi kulipia ndio maana lazima tupiganie kupata maendeleo ili tuishi maisha yenye ubora.

0766817574
Josejulius1990@gmail.com

Share this

1 Response to "PONA KWA IMANI YAKO ILA USIDANGANYIKE"

  1. Naanza kwa kutoa pongezi kwa Joseph Julius kwa kazi nzuri unayoifanya. Binafsi nadhani wakati umefika kuanza kutumia sayansi kutatua matatizo yanayotukabiri katika jamii yetu kwa kuwa teknologia imekua kwa kiwango kikubwa sana ambacho matatizo mengi yanaweza kupatiwa ufumbuzi.

    ReplyDelete