AJALI
YA KIHISTORIA: RANGI, UWEZO WA KIAKILI NA TOFAUTI YA MAENDELEO
DUNIANI
Tukiwa
tumepumzika kwenye kivuli ikiwa ni baada ya vipindi vya darasani,
tulijikuta katika mabishano ya kwa nini watu weupe wanaonekana kua
wameendelea zaidi ya weusi. Wote walikubaliana kwamba watu weupe ni
watofauti sana na ndivyo walivyozaliwa kua wenye akili na ndio
maana wao waliwahi kuendelea hata wakaja kututawala na kutufanya
watumwa. Katika lile kundi la takribani watu kumi na tano nikajikuta
ni peke yangu tu ambae nilikua kinyume nao.
Lakini
kama unavyojua, ubishi mwingi usiokua na mpangilio huwa hauangalii
nani anasema nini ila wale wenye uwezo wa kupaza sauti ya juu na
wanaokua wengi ndio huonekana wameshinda. Swali kama hili nilikua
nalo kitambo sana hata kabla ya kukutana na haya mabishano. Ni mpaka
pale nilipokutana na kitabu “Guns, Germs and Steel” ambapo
mwandishi Jared Diamonds anaonesha kwa nini sehemu nyingine zilianza
kuendelea kabla ya nyingine, ndipo angalau niliweza kujibiwa. Nami
basi mamlaka yangu atakua Jared katika kulielezea hili.
Naomba
nianze na kwa nini hawa wenzetu ni weupe kwa maksudi kabisa maana
kwenye yale mabishano yetu ya kivulini mmoja kati yetu alikwenda
mbali sana na kudiriki kusema kwamba “kile kinasaba kilichokuja na
ile rangi nyeupe ndicho pia kitakua na uwezo wa kiakili wa hawa
watu”. Lakini sayansi inatuambia sio hivyo. Tukumbuke vinasaba
vyote vya mwanadam vinajulikana ikiwa ni mafanikio ya “Human Genome
Project” iliyokamilika mwaka 2003 huko USA.
Tukumbuke
watangulizi wa wanadamu walitoka afrika. Ni pale walipoanza kjifunza
kutembea kwa miguu miwili ndipo walipoanza kuondoka afrika na kwenda
kwingineko. Rangi nyeusi ndio rangi asilia ya watangulizi wetu.
Watangulizi wetu walipoweka makazi kaskazini mwa ulaya ambako hakuna
jua la kutosha, ngozi zao hazikuweza kufyonza kiasi cha jua la
kutosha ili kupata vitamin D. Wengi walipata matatizo ya mifupa
ikiwemo matege na haikua rahisi kwao kuzaa (aidha walifariki wao
ama/na watoto wao wakati wa kujifungua ). Wakati huohuo mabadiliko
yalitokea kwenye vinasaba vinavyohusika na utoaji wa rangi nyeusi
(wanasayansi wamevigndua na kuviita SLC24A5
) na kuwapa rangi nyeupe yenye uwezo wa kuingiza kiasi kikubwa cha
jua lile chache. Kwahiyo wale waliokua wamepata mabadiliko kwenye
vinasaba hivyo waliweza kuzaa vizuri na kuendeleza uzao wakati
wengine wakitoweka, na ndio maana leo tunawaona ni weupe na sisi ni
weusi, na hakuna chochote cha kushangaza kwenye rangi yao na
aihusiani na wao kua na akili.
Picha: kuonesha kusambaa kwa watu kutoka afrika kwenda sehemu mbalimbali duniani |
Kwanini
wao waliendelea kabla yetu kiasi cha kututawala na kutufanya watumwa?
Kwanza nianze kwa kusema hata kama tutabishana kuhusu jibu la swali
hili, jibu la kwamba wao wana akili zaidi yetu hilo si kweli na
hakuna vithibitisho vya hilo. Wanaopendelea jibu hilo mara nyingi ni
wabaguzi wa rangi na wamefanikiwa kuingiza mawazo yao yasiyokua na
vithibitisho kwenye bongo za wengi ikiwemo wale wote niliojikuta nao
kivulini kwenye ubishi. Diamond anatuambia Wanasaikolojia kwenye nchi
zenye mchanganyiko wa watu weupe na weusi wametafuta kwa nguvu zote
kwa makumi ya miaka kuweza kuthibitisha kwamba watu weupe wana uwezo
mkubwa wa kiakili ukilinganisha na weusi ila wasipate wanachotafuta.
Wanawalinganisha watu bila hata kujiuliza kwamba wamekulia katika
mazingira,tamaduni na wenye elimu tofauti. Jared Diamond mwenyewe
ambae ameishi na watu wa New Guinea kwa miaka 33 akifanya tafiti zake
anaamini wazawa wa New Guinea ni wenye akili zaidi ya wazungu wenzie
kwa kuweza kuishi kwenye mazingira magum kama yale.
Kabla
ya miaka 11,000 iliyopita watu wote duniani waliishi kwa kuwinda na
kukusanya matunda na mizizi, hivyo katika kipindi hiki wote duniani
tulifanana hali. Karibia Dunia nzima leo haipo huko tena isipokua kwa
maeneo machache sana wakiwemo wahadzabe wa hapa Tanzania ambao
naamini nao kadiri muda unavyokwenda watatoka huko. Ni mpaka miaka
11,000 iliyopita ndipo tulianza kutofautiana kwa kilimo kugunduliwa
katika baadhi ya maeneo duniani. Kilimo ni muhimu katika swali letu
maana jamii Fulani ikiachana na kuwinda na kula matunda na mizizi
ikaanza kulima chakula na kukitunza kinachobaki na pia ikaanza kufuga
na wanyama, kwanza jamii hii itaongezeka katika idadi
ya watu, pili itapata maambukizi ya vijidudu vipya kutoka kwa wanyama
wanaowafuga na mimea wanayootesha; na tatu kwa wingi wa jamii hii
itawalazimu kutengeneza serikali na itakua na jeshi;watu mbalimbali
watajikita katika shughuli tofautitofauti mbali na ile ya wawindaji
na wakusanyaji ambamo wote huzunguka kutafuta chakula, katika jamii
inayolima na kufuga wengine watajihusisha na kuendeleza teknolojia na
humo zitatoka mashine kwa ajili ya kurahisisha kazi na silaha kwa
ajili ya kutawala jamii nyingine. Pia watakapoenda kukutana na jamii
nyingine ambayo ni mpya kwao wataiambukiza magonjwa ambayo wao tayari
wana kinga nayo, nayo inaweza hata kutoweka. Hivyo wataishia
kuwatawala wale ambao hawakuwa/walichelewa kuanza kilimo.
Vithibitisho vilivyopo mpaka leo vinaonesha kilimo kilianza kwa mara
ya kwanza katika maeneo matano duniani ambayo ni: kusini magharibi
mwa asia (pia hujulikana kama mashariki ya karibu); China;
Mesoamerica (yaani mexico ya kati na kusini na maeneo ya karibu na
amerika ya kati); Andes ya amerika kusini; na mashariki mwa marekani.
Lakini
hapa tumeongeza swali lingine kubwa zaidi, kwanini kilimo na ufugaji
ugunduliwe miaka11,000 iliyopita kwao kwanza na si huku? Jibu lake
sio kwa kua babu zao walikua na akili sana kuzidi babu zetu hapana
ila ni “ajali ya kihistoria” kama Diamond mwenyewe anavyoiita.
Maana yake ni kwamba ilitokea kama ajali wao wakajikuta wapo katika
maaeneo ambayo yanaruhusu kuanzisha kilimo na ufugaji tofauti na
sisi. Nitatoa mifano kadhaa:
Asia
na ulaya kwa pamoja inaitwa “Eurasia” na imeungana, ni kubwa
zaidi katika latitudo kuliko longitudo. Hii inamaanisha kuna
mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kidogo ukilinganisha na mabara
ambayo ni makubwa katika longitudo mfano afrika. Hii husaidia kuweza
kusambaa kwa urahisi kwa mimea na mifugo kutoka sehem moja kwenda
nyingine kwa sababu wanakua wamezoea mazingira yaleyale. Pia eneo
kubwa kabisa la kimediterania duniani linapatikana magharibi mwa
“Eurasia”; eneo hili lina mtawanyiko mkubwa wa mimea na wanyama,
linafaa kwa kilimo na ufugaji.
“Eurasia”
ndiko chanzo cha mazao mengi ya kilimo na wanyama wengi wanaoonekana
leo duniani wakifugwa. Kati ya mifugo mikuu mitano ya kufuga iliyopo
duniani leo, minne (ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe) ilifugwa kwa
mara ya kwanza huko na baadae kutawanywa maeneo mbalimbali duniani.
Kwa
kua chakula kilipatikana kwa wingi katika meeneo yaliyoanza kulima
hata kingine kikatunzwa. Hakukua na haja ya kila mtu kujikita katika
utafutaji wa chakula. Basi watu wakabobea katika fani mbalimbali.
Wengine wakawa viongozi wa serikali wenye kuangalia wapi pa kutawala
na kuendesha jamii kupitia kodi iliyokua ikikusanywa. Wengine wakawa
wanajeshi na kupigana katika vita vya kuyatawala maeneo mengine
yaliyokua hayajaendelea. Wenngine wakajikita na teknolojia
wakatengeneza mashine mbalimbali kama magari ya kuvutwa na farasi,
silaha zenye uwezo wa hali ya juu kama bunduki ukilinganisha na mawe
ama marungu waliokua nayo waliopambana nao. Na kikubwa zaidi
wakagundua kuandika, kitu ambacho kiliharakisha utawala wa maeneo
mapya pale walipoyaona na kuandika kuhusu taarifa zake na habari
zikawafikia wengine katika maeneo mengine.
Kuhitimisha,
ni kwamba hawa watu weupe walianza kuendelea kabla ya wengine sio kwa
sababu wao wana akili sana ama wamebarikiwa sana ila ni kama bahati
kwao kwamba walijikuta katika maeneo ambako kuna uwezekano wa
kuendelea kuliko mengine, maeneo yenye wanyama wa kufugika, yenye
mimea ya kufanyia kilimo na yenye geografia inayoruhusu. Kama
tungekua tumekwishagundua chombo chenye uwezo wa kurudi nyuma ya muda
(time machine) na tungerudi miaka 11,000 iliyopita tukabadilisha sisi
ndio tukaanza kugundua kilimo na ufugaji na wao wakaendelea kua
wawindaji na wakusanya matunda na mizizi, leo ingekua kinyume na
ilivyo. Kwa leo kila wanachoweza kufanya hata sisi tunaweza kama
tumepewa kile walichopewa ili wafanye kitu flani mfano elimu ama
mtaji. Wenzetu wanaoishi nao katika maazingira yaleyale
wamekwishatuonesha vithibitisho kwa kufanya vitu vikubwa huko kwao.
Obama, Dr. Ben Carson, Martin Luther King, Nelson Mandela, Kambarage
Nyerere, Kofi Annan, Wangari Muta Maathai, Oprah Winfrey ni mifano
michache tu.
Tujiamini
na tuongeze bidii ya kubadilisha hali ya jamii yetu, tusikubali
mawazo ya kiubaguzi wa rangi kuzama kwenye maada yenye kilo 2
iliyokaa ndani ya mafuvu yetu, uliokuwepo ni utofauti wa kimazingira
na sio vitu ambavyo vipo ndani yetu.
Joseph J. Masalu
Muhimbili University of health and allied sciences(MUHAS)
Kitu amabacho bado kinanitatiza, sasa kuna teknologia kubwa sana...na inapatika sehemu nyingi sana duniani mbona sisi bado tuko nyuma bado....au umasikini ndio tatizo kubwa?
ReplyDeletenafikiri tatizo letu kubwa sana ni umasikin na sisi tulio wengi hatuna udhubutu, nikimaanisha kuwa hatuna ile nguvu ya kujaribu kufanya mambo makubwa yanayoleta mabadiliko na pia maendeleo kati yetu....
Deleteuwezo wa kiuchumi wa wazungu ndo unatufanya tuwe mazezeta. Wanatumia mwanya wa uchumi kututawala.
ReplyDeletekama ulivyosema bwana Joseph, utofauti wetu nao sio wa kiakili ni wa kimazingira.
kuna kitabu kimoja kimeandikwa na Walter Rodney, How europe underdeveloped Afica? kinagusia san mambo hayo...
Kwa mtazamo wangu nafkiri sababu ni kutojiamini na hii inasababishwa na elimu tunayopitia na malezi tangia utotoni, tunakuzwa kwa woga, mengi tunayofanya ni sababu ya kuepuka adhabu, hatulelewi na kufundishwa kujiamini na kuwa washindani. Hadi tunapokua akili yetu inajengwa hivyo, hata kufunga mkanda tukiwa kwenye gari ni sababu ya kuogopa kukamatwa, tofauti kabisa na jinsi wenzetu wanavyofunzwa
ReplyDelete