TIBA ILIYOTUKUKA: TIBA YA KISASA NA MATUMIZI MABAYA YA TIBA MBADALA
Naandika
hapa baada ya kuona hakuna anaeandika ama kujitokeza hadharani
kuongelea kuhusu hili. Naamini kuna madaktari bingwa na wa uhakika
wenye ujuzi mkubwa katika maswala yahusuyo tiba na afya kwa ujumla
katika nchi hii; najua hawa ndio walipaswa waandike haya maana wana
ujuzi na uzoefu zaidi yangu. Ila nahisi kwa uchache wao ukilinganisha
na namba ya watu wanaohitaji huduma yao na kwa kujitolea kwao kwa
ajili ya afya ya wengine wamebanana.
Mara
kadhaa nikikaa mbele ya runinga ama kufungua redio huja vipindi
vinavyojiita ni vya “afya”. Nami kwa kua ni mwanafunzi wa
udaktari basi hujilamba midomo nisubiri elimu inayotolewa na watu
waliokwenda kwenye mfumo huu wa kisasa wa mawasiliano ili wawafikie
watanzania wengine kuwapa elimu ya afya na tiba. Hazipiti dakika
chache baada ya kuanza kipindi huwa naanza kusikia maneno ya
kuchefusha nikaukunja wangu wajihi, ila linalokuja kunitapisha huwa
ni hawa watu wanaposema wana vibali vinavyotambulika na wizara ya
afya na ustawi wa jamii.
Kwa
kuwa natambua mtu anapohitaji tiba ama elimu ya kiafya huwa ana
shida, shida hii huenda ikawa ugonjwa alionao ama kutaka kuzuia
magonjwa ambayo bado hajayapata; Basi kimbilio la mnyonge huyu huwa
ni wanaoitwa ama kujiita wataalam wa mambo ya afya ambao serikali
kupitia wizara yake ya afya na ustawi wa jamii imewathibitisha
ikawaruhusu wakaguse maisha ya watanzania. Hapa huwa siachi kufikiria
jinsi kimbilio la wanyonge linavyoweza kujigeuza nyoka kwa
kujikumbusha maneno ya mshairi T. Mvungi kwenye Mashairi ya
Chekacheka:
Kimbilio
la wanyonge, limejigeuza chatu,
Chatu
mmeza matonge, asiyeogopa watu,
Dawaye
uchonge singe, chatu afanywe si kitu,
Akishaoza
samaki, busara ni kumtupa.
Naamini
mimi ni mmoja kati ya watu wenye wajibu wa kuzichonga singe kumuokoa
mtanzania mwenzangu kwenye janga hili la hawa watu na ninafanya hivyo
kwenye haya chache zijazo:
Lakini
kabla sijaenda mbali, na isijekua namie ninavutia upande wangu,
kwanza tujiulize: NI IPI TIBA YA KWELI?
Tiba
ya kweli ni ile iliyothibitishwa kufanya kile inachodai inafanya;
iliyofanyiwa utafiti wa kina wa kisayansi usio baguzi. Hapa si tu ile
anayopewa mtu alieugua tayari ili apone pekee bali ni pamoja na
ushauri wowote wa kiafya unaotolewa (nakosa msamiati wa kuviunganisha
hivi viwili). Hii ni ile ya kisasa ila baadhi ya tiba mbadala
zimeoneshwa kuwa na vithibitisho pia, na hizi ni 1. Homeopathy
(matumizi ya vitu vinavyosababisha ugonjwa kwa kiasi kidogo sana
kutibu ugonjwa huo) 2. Osteopathy (kutibu kwa kutambua uhusiano kati
ya misuli, mifupa na afya) 3. Chiropractic (kutibu kwa kutambua
uhusiano kati ya uti wa mgongo na afya) 4. Acupuncture (kutuliza
maumivu kwa kuchomeka sindano kwenye ngozi) 5. Herbal Medicine
(mitishamba) (Davidson’s principles & practice of medicine
21st ed, 2010. Pg 15). Japo mara nyingi
jinsi zinavyofanya kazi huwa inapotoshwa na kuzielezea moja baada ya
nyingine itahitaji makala nyingine.
Acupuncture |
Wengi
wa hawa watu wanaokwenda kwenye runinga kufanya vipindi vya afya
(ambavyo kiuhalisia huwa ni matangazo yao ya biashara) huwa wanaongea
vitu wasivyovifaham kwa undani, ambavyo wana ujuzi navyo wa juu juu
sana aidha kwa kusoma kwenye mitandao ama kusikia sehemu, ila cha
muhimu kuliko yote ni kwamba havina VITHIBITISHO vya kisayansi kwa
kile wanachosema. Nakumbuka wakati nipo sekondari nilikua navutiwa
sana na habari za kisayansi, nilipenda kuzisikia ama kuziangalia
kwenye runinga nyumbani. Alikuepo bwana mmoja aliitwa Isaac Ndodi
aliekua akiendesha kipindi kilichoanza kwa nyimbo za dini na kisha
akaanza kuelezea biolojia anayojua yeye mwenyewe na jinsi gani
magonjwa yanatokea mfano alisema “kunywa maji pamoja na chakula
husababisha magonjwa”. Nilipokua kitaaluma na nikawa naangalia
nyuma niliwaza huyu bwana alikua anatoa wapi haya mambo? je alikua
anatoa malezo yoyote kwanini? Je kulikua na vithibitisho vyovyote vya
anavyodai? Na kama serikali ilimpa kibali kweli, je haifuatilii nini
anafanya? Wengine walijitokeza wakisema wana dawa za kutibu magonjwa
sugu kama kisukari, shinikizo la damu, saratani na kadhalika. Ila leo
nikiwaza hawa walitakiwa wapate tuzo za nobel kwa kazi hizo.
Wengi
wa hawa watu hupenda kuunganisha tiba zao na mambo ya kiroho.
Watakwambia mungu aliwaweka wanadam wa kwanza wale mboga na matunda
na wakaishi miaka mingi bila magonjwa; japo ukienda kwenye jamii
zilizobaki zinazokula mboga na matunda mfano wahadzabe wa hapa kwetu
utakuta wana afya mbovu zaidi yetu. Kitendo cha kuunganisha mambo ya
kiroho na tiba zao ni mbinu za kumfanya mteja wao awaamini kiasi cha
kutokuhoji kama tusivyotakiwa kuhoji mambo ya imani.
Na
watu hawa wapo kwa ajili ya watu wenye pesa kwani huduma zao ni ghali
mno tofauti na ilivyooneshwa kwenye mtandao wa Foreplan Herbal Clinic
inayomilikiwa na J.J.Mwaka ambapo wanasema wao hawapo kwa ajili ya
pesa bali huduma na mara nyingine hutoa huduma za bure kwa
wasiojiweza. Ninae rafiki yake na rafiki yangu mmoja ambae amekua
akisumbuliwa na maumivu ya mgongo kwa muda sasa na aliamua kujikita
na hizi tiba mbadala na anasema baada ya yeye kuambiwa kushika
kimtambo ambacho kinaweza “kuchunguza mwili mzima” basi
walimwambia “wamegundua ana mafuta mengi kwenye mgongo na yanazuia
damu inayopitia mgongoni isifike kwenye ubongo, hivyo ndio maana
anaumwa mgongo”. Baadae wakamuuzia dawa za kienyeji ambazo alisema
nyingine zilikua kama vumbi ambalo atakua anatia kwenye chai, na
nyingine kama kinyesi cha ng’ombe, pia wakamshauri akanunue asali
mbichi nyingi sana atumie na kwa wakati huo aache kula nyama kwani
ina mafuta. Kwa vyote hivi alitumia zaidi ya Sh. 120,000/= za
kitanzania na asione maumivu hata yakipungua wakati akikosa burudani
ya vyakula vitamu vyenye protini nyingi kama nyama na kunyweshwa
takataka asizozijua kwa dozi isiyochunguzwa madhara yake. Gharama hii
kubwa husababisha hawa jamaa waone wagonjwa wachache kwa siku
ukilinganisha na daktari wa tiba ya kisasa na ya kisayansi. Hapa
huweza kuongea na wagonjwa kwa ukaribu sana na ujaliji ambao hata
mimi ninautamani sana. Hiki ndicho huwa kinawaponya hawa wagonjwa
ikitokea wanapona ukijumlisha na ukweli kwamba mwili una uwezo wake
wa asili wa kujiponya wenyewe, na sio yale wanayoyafanya.
Ukienda
kwenye tiba ya kisasa, achilia mbali usumbufu utakaoupata mwanzoni
ili uonane na daktari pia hatoweza kukusikiliza kana kwamba upo peke
yako siku iyo bali ni watu wengi waliozidi watu anaotakiwa kuwaona
kwa siku ila nae hujitahidi kadiri awezavyo. Baada ya kukusikiliza
hukumbuka kile alichojifunza ambacho njia za kisayansi dunia nzima
zimeonesha hivyo, huja na hisia ya nini kinachokusumbua. Yeye haishii
hapa bali hutaka kuonesha vithibitisho kama kweli anachofikiria ni
sawa, na hapa atakuchukua vipimo (mfano atahitaji kujua kama kuuma
kwa tumbo lako kunasababishwa na vijidudu vilivyokuingia tumboni pale
ulipokula chakula kisicho salama, kwa kuchukua kinyesi chako na
kupeleka maabara ili wakaangalie kama hivyo vijidudu vimo maana
kinyesi kimetoka huko viliko vijidudu). Baadae akishajua nini shida
hujiuliza ni njia gani ya kutibu ugonjwa wako inayotumika kwa sasa na
ambayo imethibitishwa kisayansi na inakubalika dunia nzima. Basi
utapewa dawa ama kufanyiwa upasuaji. Dawa zetu hawa jamaa wameziita
kemikali pasi hata na kujua nini maana ya hili neon. Kemia ya kidato
cha kwanza haikueleweka vizuri hapa. Kwa maana ya kemikali, zetu ni
kemikali ila na zao ni kemikali, bila kusahau vitu vingi tu vya
asili. Lakini siku zote mambo hayawi hivi kwani si magonjwa yote
tunajua sababu zake; ila hata kama ikiwa hivyo tunakua wawazi tu na
tunasubiri tukijua tafiti zinaendelea na ipo siku watakuja na majibu
hata kama sisi tutakua hatupo.
Kwa
kuhitimisha naomba nihimize mambo kadhaa:
Kwanza
pindi tusikiapo watu wanatoa elimu za afya, tuwahoji watuelezee kwa
kina tuelewe angalau kwa ujumla, kama hawawezi kutuelezea tuelewe
basi wao wenyewe hawavielewi. Pili watupe vithibitisho vya kisayansi
kuhusu yale wanayodai, watuambie wametoa wapi wanavyosema na kama
wameota kama babu wa Loliondo basi tuwapotezee. Tatu tuwe wagumu wa
kuamini haraka kama alivyokua Tomaso mwanafunzi wa Yesu; Tukisikia
mtu anatibu saratani ama VVU/UKIMWI basi tujiulize kwa nini anakuja
kuhangaika kwenye runinga ya ndani ya nchi wakati ugonjwa huo unatesa
dunia nzima? Tujiulize kama hivyo vyakula wanavyosema vinatibu
magonjwa flani mfano tango, nyanya, ukwaju, vitunguu na vinginenyo ni
kwanini basi tunapata wakati twavila mara kwa mara? Mwisho
tuunganishe nguvu kwa pamoja katika kuhimiza umuhimu wa kujielimisha
na kukuza sekta ya afya ya kisasa maana hii ndiyo iliyoweza kuongeza
muda wa wanadamu kuishi duniani maradufu, imeupoteza ugonjwa wa Ndui
kwenye uso wa dunia kwa chanjo, imepunguza vifo vya watoto chini ya
miaka 5 ukilinganisha na zamani, na haijakaa kibiashara kwani
madaktari walio wengi huwa na wito wa kusaidia na wanaishi wakijua
hawawezi kuwa matajiri, na mengine mengi.
JOSEPH JULIUS
JOSEPH JULIUS
Serikali na Jamii kwa ujumla,inapaswa kuliangalia suala hili kwa jicho la pili.
ReplyDelete