Monday 29 September 2014

NGONO,DUNIA YA LEO NA JAMII


NGONO,DUNIA YA LEO NA JAMII
Joseph Julius MD(MUHAS)
Habarini za leo ndugu wasomaji! Kwanza nitangulize heshima zangu za dhati kwa ndugu Paschal Ndaro kwa ubunifu alio nao wa kutumia maendeleo ya teknohama kusababisha sisi kuweza kuelimishana, kubadilishana ufahamu na kuburudishana kama ilivyo hapa.
Pia niongeze kuwa kama mtu ana chochote cha kuchangia basi ni vyema tukachangia hapa hapa kwenye blogi ili kuwapanua zaidi wanaosoma. Binafsi napenda kuandika kwa lugha yetu mama ili kuwafikia wengi na pia nina wazo la kuongeza misamiati kwenye lugha yetu hii,ila kama mahitaji ya utafsiri yatajitokeza basi sintokuwa na budi kufanya hivyo.
Leo nitagusia swala nyeti sana kwenye maadili ya mwanadam; nitachambua swala la ngono katika uhusiano na maendeleo ya dunia ya leo na jamii yetu. Kabla ya yote na tutambue tofauti yetu sisi wanadam na wanyama wengine(sisi nao ni wanyama pia). Vinasaba vya binadam vinafana na vile vya sokwe kwa zaidi ya 98% na vile vya mmea wa nyanya kwa 60%,pia vipande vidogo kabisa(atomu) vinavyotuunda vinapatikana kwenye mawe,mchanga,maji na hata nyota. Kinachotutofautisha na mengine hayo yote ni tamaduni,zinazotokana na ubongo wetu kuwa mkubwa ukilinganisha na viumbe wengine.
Kila tamaduni huwa zinaweka sheria zake kuhusu swala la ngono ambazo huwa zinahusishwa na ndoa kwa upande mmoja na makatazo au ruhusa katika vipindi mbalimbali kwa upande mwingine. Binafsi nimekuzwa katika familia ya kikristu na nilifundishwa kufuata maelekezo kutoka kwenye kitabu cha biblia kwenye mambo mengi ninayofanya,hasa maadili,ninaamini pia hata wewe huwa unatumia/umewahi kutumia mafundisho ya dini yako kukuongoza katika maadili.
Kutoka 20:14 imeandika “usizini”,20:17 ikakataza hata usimtamani mke wa jirani yako,wakati katika Mathayo 5:28 Yesu anasema “lakini mimi nawaambieni,atakaemtazama mwanamke kwa kumtamani,amekwishazini naye moyoni mwake”.Kanisa katoliki likaenda mbali mpaka kuwachagulia watu jinsi ya kufanya tendo hili kwa kuweka ‘staili ya kimisionari’ ambayo ndio inakubalika. Hii sio makala ya kidini ila najaribu kuonesha vyanzo vyetu vya kujifunzia vilivyolipa uzito swala hili. Niliwahi kujifunza pia kuwa vitabu vyetu vya dini vimeandikwa katika lugha ya picha na pia viliandikwa wakati tofauti na sasa,kwa hiyo tunaweza kusoma kitu ila tukakitafsiri vingine kutokana na muda tunaoishi(mfano swala la kumiliki watumwa,wachungaji wa kike,dunia kuzunguka jua na sio kama ilivyoandikwa,n.k).
Ngono inachukua picha gani kwenye jamii katika dunia ya leo? Sio miaka mingi iliyopita ilikua ni kukosa maadili kama utaliongelea swala la ngono(hata sasa miongoni mwetu) mbele ya watu,lilionekana ni jambo nyeti linalohitaji usiri(nikiwa mdogo nilikua nikiona ng’ombe wetu wanapanda niliambiwa wanacheza). Huko Marekani pia hali ilikua hivyo mpaka miaka ya 1940 na 1950 ambapo Alfred C.Kinsey alipofanya utafiti wa kisayansi kuhusu ngono na vitendo vinavyohusiana na ngono kwa wanadam. Kwa mara ya kwanza wamarekani walijifunza kua: zaidi ya 90% ya vijana wao wamewahi kupiga punyeto,10% walikua ni mashoga, wasichana nao huwa wanafika kileleni,na pia wasagaji wana ufanisi mkubwa wa kuwafikisha kileleni wasichana zaidi ya wavulana wanavyoweza. Kinsley alilaumiwa sana kwa kukosa maadili lakini utafiti wake ulisaidia watu kujitambua zaidi na kuboresha maisha yao ya mapenzi.
Hatutakiwi kabisa kulionea aibu swala la ngono. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na idara ya magonjwa ya akili katika chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi (MUHAS) ulionesha kua 10% ya watoto kati ya umri wa miaka 12 hadi 14 wamewahi kufanya ngono,na miongoni mwao 68% hawakutumia mpira. Tukinyamaza,hawa watoto watapata madhara kwa kua hawajui nini kipo mbele yao.
Tukisikia kuwaka tamaa za ngono wala tusisikitike maana sayansi inatueleza kua sababu zake ni nzuri tu,sawa na zile sababu za kusikia njaa au kiu au maumivu. Asilia inatutengeneza kuhakikisha tunapeleka nakala ya vinasaba vyetu kwenye vizazi vijavyo kupitia kuzaliana,na tutafanya hivyo tukiwa tumekwishapevuka;na tukishapevuka asilia haina tena kazi na sisi na inatuacha tuzeeke mpaka tufe,yenyewe haijali. Tumetengenezwa na kemikali(homoni) ambazo zikitoka sisi sio wa kuamua tena ila ni kutamani tu,kemikali hizi zipo kwa wingi kwa wanaume zaidi ya wanawake na ndio maana wanaume wanatamani zaidi. Tofauti yetu wanadam na wanyama wengine ni kua sio lazima tufuate asilia inachotaka,ndio maana kuna maseja na sio kila tukijisikia kutamani tunafanya,tuna mipango.
Ule wakati wa kuwaona watu wanaofanya ngono kama wanakosea sana mi naona umepita,lakini pia ngono isitumike kama chanzo cha ukandamizaji na uonevu au kutaka kujipatia vitu kama mrejesho,heshima iwepo. Ule wakati wa watu kusubiri mpaka ndoa nao umepita maana kitendo ni kilekile. Ule wakati wa kuoneana aibu kuzungumzia maswala ya muhimu kama ngono kwenye jamii zetu nao umepita kwa maana leo kuna magonjwa ya zinaa na kupanga uzazi,lazima tuyaelewe. Na tuache kuweka matabaka ya kimaadili kwa kuwaona watu wengine wasafi na kuwasema wengine hawajatulia kisa tu wanashiriki tendo kabla hawajaoana,swala hili ni binafsi (labda hao wasafi wanaridhika na punyeto,ambayo sio mbaya japo watu hawapendi kujulikana kua huwa wanafanya),na mwisho watu wawili waliokubaliana mambo yao sisi inatuhusu nini na hawatuumizi lolote?sisi ni mapolisi wa maadili?tupanue wigo wa kuyaangalia maadili kwa kuelewa vitu kwa undani wake.

Share this

4 Responses to "NGONO,DUNIA YA LEO NA JAMII"

  1. Ni kweli mambo haya sio ya kuonea aibu tena hasa katika kipindi hiki.Ni vizuri elimu ya uzazi itolewe kwa watoto wanapofikisha umri wa kubalehe waweze kufahamu mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika kipindi hicho katika miili yao,hii itasaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa hasa UKIMWI.
    Lakini pia ni muhimu mtoto kukuzwa katika maadili mazuri,ikijumuisha na elimu aliyoipata matokeo yatakuwa mazuri.

    ReplyDelete
  2. Napenda unavyofikiria,utamaduni Ni kitu kizuri ila unaweka mipaka ya watu kufikiria nje na zaidi....vipaji vingi vinapotea kwa sababu ya mipaka hyo....wajasili wachache ndo wanaweza kuivuka na kufanya kile kilichoko kwenye akili zao

    ReplyDelete
  3. Ahsante Joseph Julius MD kwa kuonesha njia.. Tuko pamoja katika kufanikisha mabadiliko katika jamii...!

    ReplyDelete