Tuesday 20 October 2015

TIBA ILIYOTUKUKA: TIBA YA KISASA NA MATUMIZI MABAYA YA TIBA MBADALA


 TIBA ILIYOTUKUKA: TIBA YA KISASA NA MATUMIZI MABAYA YA TIBA MBADALA
Naandika hapa baada ya kuona hakuna anaeandika ama kujitokeza hadharani kuongelea kuhusu hili. Naamini kuna madaktari bingwa na wa uhakika wenye ujuzi mkubwa katika maswala yahusuyo tiba na afya kwa ujumla katika nchi hii; najua hawa ndio walipaswa waandike haya maana wana ujuzi na uzoefu zaidi yangu. Ila nahisi kwa uchache wao ukilinganisha na namba ya watu wanaohitaji huduma yao na kwa kujitolea kwao kwa ajili ya afya ya wengine wamebanana.
Mara kadhaa nikikaa mbele ya runinga ama kufungua redio huja vipindi vinavyojiita ni vya “afya”. Nami kwa kua ni mwanafunzi wa udaktari basi hujilamba midomo nisubiri elimu inayotolewa na watu waliokwenda kwenye mfumo huu wa kisasa wa mawasiliano ili wawafikie watanzania wengine kuwapa elimu ya afya na tiba. Hazipiti dakika chache baada ya kuanza kipindi huwa naanza kusikia maneno ya kuchefusha nikaukunja wangu wajihi, ila linalokuja kunitapisha huwa ni hawa watu wanaposema wana vibali vinavyotambulika na wizara ya afya na ustawi wa jamii.
Kwa kuwa natambua mtu anapohitaji tiba ama elimu ya kiafya huwa ana shida, shida hii huenda ikawa ugonjwa alionao ama kutaka kuzuia magonjwa ambayo bado hajayapata; Basi kimbilio la mnyonge huyu huwa ni wanaoitwa ama kujiita wataalam wa mambo ya afya ambao serikali kupitia wizara yake ya afya na ustawi wa jamii imewathibitisha ikawaruhusu wakaguse maisha ya watanzania. Hapa huwa siachi kufikiria jinsi kimbilio la wanyonge linavyoweza kujigeuza nyoka kwa kujikumbusha maneno ya mshairi T. Mvungi kwenye Mashairi ya Chekacheka:
Kimbilio la wanyonge, limejigeuza chatu,
Chatu mmeza matonge, asiyeogopa watu,
Dawaye uchonge singe, chatu afanywe si kitu,
Akishaoza samaki, busara ni kumtupa.
Naamini mimi ni mmoja kati ya watu wenye wajibu wa kuzichonga singe kumuokoa mtanzania mwenzangu kwenye janga hili la hawa watu na ninafanya hivyo kwenye haya chache zijazo:
Lakini kabla sijaenda mbali, na isijekua namie ninavutia upande wangu, kwanza tujiulize: NI IPI TIBA YA KWELI?
Tiba ya kweli ni ile iliyothibitishwa kufanya kile inachodai inafanya; iliyofanyiwa utafiti wa kina wa kisayansi usio baguzi. Hapa si tu ile anayopewa mtu alieugua tayari ili apone pekee bali ni pamoja na ushauri wowote wa kiafya unaotolewa (nakosa msamiati wa kuviunganisha hivi viwili). Hii ni ile ya kisasa ila baadhi ya tiba mbadala zimeoneshwa kuwa na vithibitisho pia, na hizi ni 1. Homeopathy (matumizi ya vitu vinavyosababisha ugonjwa kwa kiasi kidogo sana kutibu ugonjwa huo) 2. Osteopathy (kutibu kwa kutambua uhusiano kati ya misuli, mifupa na afya) 3. Chiropractic (kutibu kwa kutambua uhusiano kati ya uti wa mgongo na afya) 4. Acupuncture (kutuliza maumivu kwa kuchomeka sindano kwenye ngozi) 5. Herbal Medicine (mitishamba) (Davidson’s principles & practice of medicine 21st ed, 2010. Pg 15). Japo mara nyingi jinsi zinavyofanya kazi huwa inapotoshwa na kuzielezea moja baada ya nyingine itahitaji makala nyingine.
Acupuncture

Wengi wa hawa watu wanaokwenda kwenye runinga kufanya vipindi vya afya (ambavyo kiuhalisia huwa ni matangazo yao ya biashara) huwa wanaongea vitu wasivyovifaham kwa undani, ambavyo wana ujuzi navyo wa juu juu sana aidha kwa kusoma kwenye mitandao ama kusikia sehemu, ila cha muhimu kuliko yote ni kwamba havina VITHIBITISHO vya kisayansi kwa kile wanachosema. Nakumbuka wakati nipo sekondari nilikua navutiwa sana na habari za kisayansi, nilipenda kuzisikia ama kuziangalia kwenye runinga nyumbani. Alikuepo bwana mmoja aliitwa Isaac Ndodi aliekua akiendesha kipindi kilichoanza kwa nyimbo za dini na kisha akaanza kuelezea biolojia anayojua yeye mwenyewe na jinsi gani magonjwa yanatokea mfano alisema “kunywa maji pamoja na chakula husababisha magonjwa”. Nilipokua kitaaluma na nikawa naangalia nyuma niliwaza huyu bwana alikua anatoa wapi haya mambo? je alikua anatoa malezo yoyote kwanini? Je kulikua na vithibitisho vyovyote vya anavyodai? Na kama serikali ilimpa kibali kweli, je haifuatilii nini anafanya? Wengine walijitokeza wakisema wana dawa za kutibu magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu, saratani na kadhalika. Ila leo nikiwaza hawa walitakiwa wapate tuzo za nobel kwa kazi hizo.





Wengi wa hawa watu hupenda kuunganisha tiba zao na mambo ya kiroho. Watakwambia mungu aliwaweka wanadam wa kwanza wale mboga na matunda na wakaishi miaka mingi bila magonjwa; japo ukienda kwenye jamii zilizobaki zinazokula mboga na matunda mfano wahadzabe wa hapa kwetu utakuta wana afya mbovu zaidi yetu. Kitendo cha kuunganisha mambo ya kiroho na tiba zao ni mbinu za kumfanya mteja wao awaamini kiasi cha kutokuhoji kama tusivyotakiwa kuhoji mambo ya imani.
Na watu hawa wapo kwa ajili ya watu wenye pesa kwani huduma zao ni ghali mno tofauti na ilivyooneshwa kwenye mtandao wa Foreplan Herbal Clinic inayomilikiwa na J.J.Mwaka ambapo wanasema wao hawapo kwa ajili ya pesa bali huduma na mara nyingine hutoa huduma za bure kwa wasiojiweza. Ninae rafiki yake na rafiki yangu mmoja ambae amekua akisumbuliwa na maumivu ya mgongo kwa muda sasa na aliamua kujikita na hizi tiba mbadala na anasema baada ya yeye kuambiwa kushika kimtambo ambacho kinaweza “kuchunguza mwili mzima” basi walimwambia “wamegundua ana mafuta mengi kwenye mgongo na yanazuia damu inayopitia mgongoni isifike kwenye ubongo, hivyo ndio maana anaumwa mgongo”. Baadae wakamuuzia dawa za kienyeji ambazo alisema nyingine zilikua kama vumbi ambalo atakua anatia kwenye chai, na nyingine kama kinyesi cha ng’ombe, pia wakamshauri akanunue asali mbichi nyingi sana atumie na kwa wakati huo aache kula nyama kwani ina mafuta. Kwa vyote hivi alitumia zaidi ya Sh. 120,000/= za kitanzania na asione maumivu hata yakipungua wakati akikosa burudani ya vyakula vitamu vyenye protini nyingi kama nyama na kunyweshwa takataka asizozijua kwa dozi isiyochunguzwa madhara yake. Gharama hii kubwa husababisha hawa jamaa waone wagonjwa wachache kwa siku ukilinganisha na daktari wa tiba ya kisasa na ya kisayansi. Hapa huweza kuongea na wagonjwa kwa ukaribu sana na ujaliji ambao hata mimi ninautamani sana. Hiki ndicho huwa kinawaponya hawa wagonjwa ikitokea wanapona ukijumlisha na ukweli kwamba mwili una uwezo wake wa asili wa kujiponya wenyewe, na sio yale wanayoyafanya.
Ukienda kwenye tiba ya kisasa, achilia mbali usumbufu utakaoupata mwanzoni ili uonane na daktari pia hatoweza kukusikiliza kana kwamba upo peke yako siku iyo bali ni watu wengi waliozidi watu anaotakiwa kuwaona kwa siku ila nae hujitahidi kadiri awezavyo. Baada ya kukusikiliza hukumbuka kile alichojifunza ambacho njia za kisayansi dunia nzima zimeonesha hivyo, huja na hisia ya nini kinachokusumbua. Yeye haishii hapa bali hutaka kuonesha vithibitisho kama kweli anachofikiria ni sawa, na hapa atakuchukua vipimo (mfano atahitaji kujua kama kuuma kwa tumbo lako kunasababishwa na vijidudu vilivyokuingia tumboni pale ulipokula chakula kisicho salama, kwa kuchukua kinyesi chako na kupeleka maabara ili wakaangalie kama hivyo vijidudu vimo maana kinyesi kimetoka huko viliko vijidudu). Baadae akishajua nini shida hujiuliza ni njia gani ya kutibu ugonjwa wako inayotumika kwa sasa na ambayo imethibitishwa kisayansi na inakubalika dunia nzima. Basi utapewa dawa ama kufanyiwa upasuaji. Dawa zetu hawa jamaa wameziita kemikali pasi hata na kujua nini maana ya hili neon. Kemia ya kidato cha kwanza haikueleweka vizuri hapa. Kwa maana ya kemikali, zetu ni kemikali ila na zao ni kemikali, bila kusahau vitu vingi tu vya asili. Lakini siku zote mambo hayawi hivi kwani si magonjwa yote tunajua sababu zake; ila hata kama ikiwa hivyo tunakua wawazi tu na tunasubiri tukijua tafiti zinaendelea na ipo siku watakuja na majibu hata kama sisi tutakua hatupo.
Kwa kuhitimisha naomba nihimize mambo kadhaa:
Kwanza pindi tusikiapo watu wanatoa elimu za afya, tuwahoji watuelezee kwa kina tuelewe angalau kwa ujumla, kama hawawezi kutuelezea tuelewe basi wao wenyewe hawavielewi. Pili watupe vithibitisho vya kisayansi kuhusu yale wanayodai, watuambie wametoa wapi wanavyosema na kama wameota kama babu wa Loliondo basi tuwapotezee. Tatu tuwe wagumu wa kuamini haraka kama alivyokua Tomaso mwanafunzi wa Yesu; Tukisikia mtu anatibu saratani ama VVU/UKIMWI basi tujiulize kwa nini anakuja kuhangaika kwenye runinga ya ndani ya nchi wakati ugonjwa huo unatesa dunia nzima? Tujiulize kama hivyo vyakula wanavyosema vinatibu magonjwa flani mfano tango, nyanya, ukwaju, vitunguu na vinginenyo ni kwanini basi tunapata wakati twavila mara kwa mara? Mwisho tuunganishe nguvu kwa pamoja katika kuhimiza umuhimu wa kujielimisha na kukuza sekta ya afya ya kisasa maana hii ndiyo iliyoweza kuongeza muda wa wanadamu kuishi duniani maradufu, imeupoteza ugonjwa wa Ndui kwenye uso wa dunia kwa chanjo, imepunguza vifo vya watoto chini ya miaka 5 ukilinganisha na zamani, na haijakaa kibiashara kwani madaktari walio wengi huwa na wito wa kusaidia na wanaishi wakijua hawawezi kuwa matajiri, na mengine mengi.

JOSEPH JULIUS


Share this

1 Response to "TIBA ILIYOTUKUKA: TIBA YA KISASA NA MATUMIZI MABAYA YA TIBA MBADALA"

  1. Serikali na Jamii kwa ujumla,inapaswa kuliangalia suala hili kwa jicho la pili.

    ReplyDelete