Friday 14 August 2015

AJALI YA KIHISTORIA: RANGI, UWEZO WA KIAKILI NA TOFAUTI YA MAENDELEO DUNIANI


 
AJALI YA KIHISTORIA: RANGI, UWEZO WA KIAKILI NA TOFAUTI YA MAENDELEO DUNIANI

Tukiwa tumepumzika kwenye kivuli ikiwa ni baada ya vipindi vya darasani, tulijikuta katika mabishano ya kwa nini watu weupe wanaonekana kua wameendelea zaidi ya weusi. Wote walikubaliana kwamba watu weupe ni watofauti sana na ndivyo walivyozaliwa kua wenye akili na ndio maana wao waliwahi kuendelea hata wakaja kututawala na kutufanya watumwa. Katika lile kundi la takribani watu kumi na tano nikajikuta ni peke yangu tu ambae nilikua kinyume nao.
Lakini kama unavyojua, ubishi mwingi usiokua na mpangilio huwa hauangalii nani anasema nini ila wale wenye uwezo wa kupaza sauti ya juu na wanaokua wengi ndio huonekana wameshinda. Swali kama hili nilikua nalo kitambo sana hata kabla ya kukutana na haya mabishano. Ni mpaka pale nilipokutana na kitabu “Guns, Germs and Steel” ambapo mwandishi Jared Diamonds anaonesha kwa nini sehemu nyingine zilianza kuendelea kabla ya nyingine, ndipo angalau niliweza kujibiwa. Nami basi mamlaka yangu atakua Jared katika kulielezea hili.
Naomba nianze na kwa nini hawa wenzetu ni weupe kwa maksudi kabisa maana kwenye yale mabishano yetu ya kivulini mmoja kati yetu alikwenda mbali sana na kudiriki kusema kwamba “kile kinasaba kilichokuja na ile rangi nyeupe ndicho pia kitakua na uwezo wa kiakili wa hawa watu”. Lakini sayansi inatuambia sio hivyo. Tukumbuke vinasaba vyote vya mwanadam vinajulikana ikiwa ni mafanikio ya “Human Genome Project” iliyokamilika mwaka 2003 huko USA.
Tukumbuke watangulizi wa wanadamu walitoka afrika. Ni pale walipoanza kjifunza kutembea kwa miguu miwili ndipo walipoanza kuondoka afrika na kwenda kwingineko. Rangi nyeusi ndio rangi asilia ya watangulizi wetu. Watangulizi wetu walipoweka makazi kaskazini mwa ulaya ambako hakuna jua la kutosha, ngozi zao hazikuweza kufyonza kiasi cha jua la kutosha ili kupata vitamin D. Wengi walipata matatizo ya mifupa ikiwemo matege na haikua rahisi kwao kuzaa (aidha walifariki wao ama/na watoto wao wakati wa kujifungua ). Wakati huohuo mabadiliko yalitokea kwenye vinasaba vinavyohusika na utoaji wa rangi nyeusi (wanasayansi wamevigndua na kuviita SLC24A5 ) na kuwapa rangi nyeupe yenye uwezo wa kuingiza kiasi kikubwa cha jua lile chache. Kwahiyo wale waliokua wamepata mabadiliko kwenye vinasaba hivyo waliweza kuzaa vizuri na kuendeleza uzao wakati wengine wakitoweka, na ndio maana leo tunawaona ni weupe na sisi ni weusi, na hakuna chochote cha kushangaza kwenye rangi yao na aihusiani na wao kua na akili.
Picha: kuonesha kusambaa kwa watu kutoka afrika kwenda sehemu mbalimbali duniani
 
Kwanini wao waliendelea kabla yetu kiasi cha kututawala na kutufanya watumwa? Kwanza nianze kwa kusema hata kama tutabishana kuhusu jibu la swali hili, jibu la kwamba wao wana akili zaidi yetu hilo si kweli na hakuna vithibitisho vya hilo. Wanaopendelea jibu hilo mara nyingi ni wabaguzi wa rangi na wamefanikiwa kuingiza mawazo yao yasiyokua na vithibitisho kwenye bongo za wengi ikiwemo wale wote niliojikuta nao kivulini kwenye ubishi. Diamond anatuambia Wanasaikolojia kwenye nchi zenye mchanganyiko wa watu weupe na weusi wametafuta kwa nguvu zote kwa makumi ya miaka kuweza kuthibitisha kwamba watu weupe wana uwezo mkubwa wa kiakili ukilinganisha na weusi ila wasipate wanachotafuta. Wanawalinganisha watu bila hata kujiuliza kwamba wamekulia katika mazingira,tamaduni na wenye elimu tofauti. Jared Diamond mwenyewe ambae ameishi na watu wa New Guinea kwa miaka 33 akifanya tafiti zake anaamini wazawa wa New Guinea ni wenye akili zaidi ya wazungu wenzie kwa kuweza kuishi kwenye mazingira magum kama yale.
Kabla ya miaka 11,000 iliyopita watu wote duniani waliishi kwa kuwinda na kukusanya matunda na mizizi, hivyo katika kipindi hiki wote duniani tulifanana hali. Karibia Dunia nzima leo haipo huko tena isipokua kwa maeneo machache sana wakiwemo wahadzabe wa hapa Tanzania ambao naamini nao kadiri muda unavyokwenda watatoka huko. Ni mpaka miaka 11,000 iliyopita ndipo tulianza kutofautiana kwa kilimo kugunduliwa katika baadhi ya maeneo duniani. Kilimo ni muhimu katika swali letu maana jamii Fulani ikiachana na kuwinda na kula matunda na mizizi ikaanza kulima chakula na kukitunza kinachobaki na pia ikaanza kufuga na wanyama, kwanza jamii hii itaongezeka katika idadi ya watu, pili itapata maambukizi ya vijidudu vipya kutoka kwa wanyama wanaowafuga na mimea wanayootesha; na tatu kwa wingi wa jamii hii itawalazimu kutengeneza serikali na itakua na jeshi;watu mbalimbali watajikita katika shughuli tofautitofauti mbali na ile ya wawindaji na wakusanyaji ambamo wote huzunguka kutafuta chakula, katika jamii inayolima na kufuga wengine watajihusisha na kuendeleza teknolojia na humo zitatoka mashine kwa ajili ya kurahisisha kazi na silaha kwa ajili ya kutawala jamii nyingine. Pia watakapoenda kukutana na jamii nyingine ambayo ni mpya kwao wataiambukiza magonjwa ambayo wao tayari wana kinga nayo, nayo inaweza hata kutoweka. Hivyo wataishia kuwatawala wale ambao hawakuwa/walichelewa kuanza kilimo. Vithibitisho vilivyopo mpaka leo vinaonesha kilimo kilianza kwa mara ya kwanza katika maeneo matano duniani ambayo ni: kusini magharibi mwa asia (pia hujulikana kama mashariki ya karibu); China; Mesoamerica (yaani mexico ya kati na kusini na maeneo ya karibu na amerika ya kati); Andes ya amerika kusini; na mashariki mwa marekani.
Lakini hapa tumeongeza swali lingine kubwa zaidi, kwanini kilimo na ufugaji ugunduliwe miaka11,000 iliyopita kwao kwanza na si huku? Jibu lake sio kwa kua babu zao walikua na akili sana kuzidi babu zetu hapana ila ni “ajali ya kihistoria” kama Diamond mwenyewe anavyoiita. Maana yake ni kwamba ilitokea kama ajali wao wakajikuta wapo katika maaeneo ambayo yanaruhusu kuanzisha kilimo na ufugaji tofauti na sisi. Nitatoa mifano kadhaa:
Asia na ulaya kwa pamoja inaitwa “Eurasia” na imeungana, ni kubwa zaidi katika latitudo kuliko longitudo. Hii inamaanisha kuna mabadiliko ya tabia nchi kwa kiasi kidogo ukilinganisha na mabara ambayo ni makubwa katika longitudo mfano afrika. Hii husaidia kuweza kusambaa kwa urahisi kwa mimea na mifugo kutoka sehem moja kwenda nyingine kwa sababu wanakua wamezoea mazingira yaleyale. Pia eneo kubwa kabisa la kimediterania duniani linapatikana magharibi mwa “Eurasia”; eneo hili lina mtawanyiko mkubwa wa mimea na wanyama, linafaa kwa kilimo na ufugaji.
Eurasia” ndiko chanzo cha mazao mengi ya kilimo na wanyama wengi wanaoonekana leo duniani wakifugwa. Kati ya mifugo mikuu mitano ya kufuga iliyopo duniani leo, minne (ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe) ilifugwa kwa mara ya kwanza huko na baadae kutawanywa maeneo mbalimbali duniani.
Kwa kua chakula kilipatikana kwa wingi katika meeneo yaliyoanza kulima hata kingine kikatunzwa. Hakukua na haja ya kila mtu kujikita katika utafutaji wa chakula. Basi watu wakabobea katika fani mbalimbali. Wengine wakawa viongozi wa serikali wenye kuangalia wapi pa kutawala na kuendesha jamii kupitia kodi iliyokua ikikusanywa. Wengine wakawa wanajeshi na kupigana katika vita vya kuyatawala maeneo mengine yaliyokua hayajaendelea. Wenngine wakajikita na teknolojia wakatengeneza mashine mbalimbali kama magari ya kuvutwa na farasi, silaha zenye uwezo wa hali ya juu kama bunduki ukilinganisha na mawe ama marungu waliokua nayo waliopambana nao. Na kikubwa zaidi wakagundua kuandika, kitu ambacho kiliharakisha utawala wa maeneo mapya pale walipoyaona na kuandika kuhusu taarifa zake na habari zikawafikia wengine katika maeneo mengine.
Kuhitimisha, ni kwamba hawa watu weupe walianza kuendelea kabla ya wengine sio kwa sababu wao wana akili sana ama wamebarikiwa sana ila ni kama bahati kwao kwamba walijikuta katika maeneo ambako kuna uwezekano wa kuendelea kuliko mengine, maeneo yenye wanyama wa kufugika, yenye mimea ya kufanyia kilimo na yenye geografia inayoruhusu. Kama tungekua tumekwishagundua chombo chenye uwezo wa kurudi nyuma ya muda (time machine) na tungerudi miaka 11,000 iliyopita tukabadilisha sisi ndio tukaanza kugundua kilimo na ufugaji na wao wakaendelea kua wawindaji na wakusanya matunda na mizizi, leo ingekua kinyume na ilivyo. Kwa leo kila wanachoweza kufanya hata sisi tunaweza kama tumepewa kile walichopewa ili wafanye kitu flani mfano elimu ama mtaji. Wenzetu wanaoishi nao katika maazingira yaleyale wamekwishatuonesha vithibitisho kwa kufanya vitu vikubwa huko kwao. Obama, Dr. Ben Carson, Martin Luther King, Nelson Mandela, Kambarage Nyerere, Kofi Annan, Wangari Muta Maathai, Oprah Winfrey ni mifano michache tu.

Tujiamini na tuongeze bidii ya kubadilisha hali ya jamii yetu, tusikubali mawazo ya kiubaguzi wa rangi kuzama kwenye maada yenye kilo 2 iliyokaa ndani ya mafuvu yetu, uliokuwepo ni utofauti wa kimazingira na sio vitu ambavyo vipo ndani yetu. 

Joseph J. Masalu
Muhimbili University of health and allied sciences(MUHAS)