NGONO,DUNIA
YA LEO NA JAMII
Joseph Julius MD(MUHAS)
Habarini za leo ndugu
wasomaji! Kwanza nitangulize heshima zangu za dhati kwa ndugu Paschal
Ndaro kwa ubunifu alio nao wa kutumia maendeleo ya teknohama
kusababisha sisi kuweza kuelimishana, kubadilishana ufahamu na
kuburudishana kama ilivyo hapa.
Pia niongeze kuwa kama
mtu ana chochote cha kuchangia basi ni vyema tukachangia hapa hapa
kwenye blogi ili kuwapanua zaidi wanaosoma. Binafsi napenda kuandika
kwa lugha yetu mama ili kuwafikia wengi na pia nina
wazo la kuongeza misamiati kwenye lugha yetu hii,ila kama mahitaji ya
utafsiri yatajitokeza basi sintokuwa na budi kufanya hivyo.
Leo nitagusia swala
nyeti sana kwenye maadili ya mwanadam; nitachambua swala la ngono
katika uhusiano na maendeleo ya dunia ya leo na jamii yetu. Kabla ya
yote na tutambue tofauti yetu sisi wanadam na wanyama wengine(sisi
nao ni wanyama pia). Vinasaba vya binadam vinafana na vile vya sokwe
kwa zaidi ya 98% na vile vya mmea wa nyanya kwa 60%,pia vipande
vidogo kabisa(atomu) vinavyotuunda vinapatikana kwenye
mawe,mchanga,maji na hata nyota. Kinachotutofautisha na mengine hayo
yote ni tamaduni,zinazotokana
na ubongo wetu kuwa mkubwa ukilinganisha na viumbe wengine.
Kila tamaduni huwa
zinaweka sheria zake kuhusu swala la ngono ambazo huwa zinahusishwa
na ndoa kwa upande mmoja na makatazo au ruhusa katika vipindi
mbalimbali kwa upande mwingine. Binafsi nimekuzwa katika familia ya
kikristu na nilifundishwa kufuata maelekezo kutoka kwenye kitabu cha
biblia kwenye mambo mengi ninayofanya,hasa maadili,ninaamini pia hata
wewe huwa unatumia/umewahi kutumia mafundisho ya dini yako kukuongoza
katika maadili.
Kutoka 20:14 imeandika
“usizini”,20:17 ikakataza hata usimtamani mke wa jirani
yako,wakati katika Mathayo 5:28 Yesu anasema “lakini mimi
nawaambieni,atakaemtazama mwanamke kwa kumtamani,amekwishazini naye
moyoni mwake”.Kanisa katoliki likaenda mbali mpaka kuwachagulia
watu jinsi ya kufanya tendo hili kwa kuweka ‘staili ya kimisionari’
ambayo ndio inakubalika. Hii sio makala ya kidini ila najaribu
kuonesha vyanzo vyetu vya kujifunzia vilivyolipa uzito swala hili.
Niliwahi kujifunza pia kuwa vitabu vyetu vya dini vimeandikwa katika
lugha ya picha na pia viliandikwa wakati tofauti na sasa,kwa hiyo
tunaweza kusoma kitu ila tukakitafsiri vingine kutokana na muda
tunaoishi(mfano swala la kumiliki watumwa,wachungaji wa kike,dunia
kuzunguka jua na sio kama ilivyoandikwa,n.k).
Ngono inachukua picha
gani kwenye jamii katika dunia ya leo? Sio miaka mingi iliyopita
ilikua ni kukosa maadili kama utaliongelea swala la ngono(hata sasa
miongoni mwetu) mbele ya watu,lilionekana ni jambo nyeti linalohitaji
usiri(nikiwa mdogo nilikua nikiona ng’ombe wetu wanapanda
niliambiwa wanacheza). Huko Marekani pia hali ilikua hivyo mpaka
miaka ya 1940 na 1950 ambapo Alfred C.Kinsey alipofanya utafiti wa
kisayansi kuhusu ngono na vitendo vinavyohusiana na ngono kwa
wanadam. Kwa mara ya kwanza wamarekani walijifunza kua: zaidi ya 90%
ya vijana wao wamewahi kupiga punyeto,10% walikua ni mashoga,
wasichana nao huwa wanafika kileleni,na pia wasagaji wana ufanisi
mkubwa wa kuwafikisha kileleni wasichana zaidi ya wavulana
wanavyoweza. Kinsley alilaumiwa sana kwa kukosa maadili lakini
utafiti wake ulisaidia watu kujitambua zaidi na kuboresha maisha yao
ya mapenzi.
Hatutakiwi kabisa
kulionea aibu swala la ngono. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na
idara ya magonjwa ya akili katika chuo kikuu cha afya na sayansi
shirikishi (MUHAS) ulionesha kua 10% ya watoto kati ya umri wa miaka
12 hadi 14 wamewahi kufanya ngono,na miongoni mwao 68% hawakutumia
mpira. Tukinyamaza,hawa watoto watapata madhara kwa kua hawajui nini
kipo mbele yao.
Tukisikia kuwaka tamaa
za ngono wala tusisikitike maana sayansi inatueleza kua sababu zake
ni nzuri tu,sawa na zile sababu za kusikia njaa au kiu au maumivu.
Asilia inatutengeneza kuhakikisha tunapeleka nakala ya vinasaba vyetu
kwenye vizazi vijavyo kupitia kuzaliana,na tutafanya hivyo tukiwa
tumekwishapevuka;na tukishapevuka asilia haina tena kazi na sisi na
inatuacha tuzeeke mpaka tufe,yenyewe haijali. Tumetengenezwa na
kemikali(homoni) ambazo zikitoka sisi sio wa kuamua tena ila ni
kutamani tu,kemikali hizi zipo kwa wingi kwa wanaume zaidi ya
wanawake na ndio maana wanaume wanatamani zaidi. Tofauti yetu wanadam
na wanyama wengine ni kua sio lazima tufuate asilia inachotaka,ndio
maana kuna maseja na sio kila tukijisikia kutamani tunafanya,tuna
mipango.
Ule wakati wa kuwaona
watu wanaofanya ngono kama wanakosea sana mi naona umepita,lakini pia
ngono isitumike kama chanzo cha ukandamizaji na uonevu au kutaka
kujipatia vitu kama mrejesho,heshima iwepo. Ule wakati wa watu
kusubiri mpaka ndoa nao umepita maana kitendo ni kilekile. Ule wakati
wa kuoneana aibu kuzungumzia maswala ya muhimu kama ngono kwenye
jamii zetu nao umepita kwa maana leo kuna magonjwa ya zinaa na
kupanga uzazi,lazima tuyaelewe. Na tuache kuweka matabaka ya
kimaadili kwa kuwaona watu wengine wasafi na kuwasema wengine
hawajatulia kisa tu wanashiriki tendo kabla hawajaoana,swala hili ni
binafsi (labda hao wasafi wanaridhika na punyeto,ambayo sio mbaya
japo watu hawapendi kujulikana kua huwa wanafanya),na mwisho watu
wawili waliokubaliana mambo yao sisi inatuhusu nini na hawatuumizi
lolote?sisi ni mapolisi wa maadili?tupanue wigo wa kuyaangalia
maadili kwa kuelewa vitu kwa undani wake.